Meneja wa klabu ya Arsenal, Arsene Wenger hii leo ametimiza miaka
18 kamili tangu alipoanza kuitumikia klabu hiyo ya kaskazini mwa jijini London
oktoba mosi mwaka 1996.
Wenger, anatimiza miaka 18 huku hii leo kikosi chake
kikikabiliwa na mchezo wa ligi ya mabingwa barani Ulaya dhidi ya Galatasaray
kutoka nchini Urutuki ambapo itamlazimu kufanya jitihada za kuinogesha furaha
ya kuwa klabuni hapo kwa muda mrefu kwa kikosi chake kusaka ushindi.
Uwepo wa meneja huyo kutoka nchini Ufaransa, unaendelea kumpa
sifa ya tofauti katika ligi ya nchini Uingereza kutokana na kuwa mtu aliyedumu
kibaruani kwa kipindi kirefu huku klabu nyingine zikifanya mabadiliko ya mara
kwa mara katika mabenchi yao ya ufundi.
Tangu mwaka 1996 Arsene Wenger, akiwa meneja wa klabu ya Arsenal
klabu nyingine 43 zilizoshiriki ligi tangu kipindi hicho zimebadilisha jumla ya
mameneja 207 na kumuacha akiwa meneja pekee anaebaki kuwa kiongozi wa benchi la
ufundi la The Gunners.
Kwa mantiki hiyo sasa Arsene Wenger, anaendelea kuwa meneja
aliyedumu Arsenal kwa kipindi kirefu kuliko meneja mwingine yoyote aliyepita
klabuni hapo na pia anakuwa meneja aliyekaa kwa kipindi kirefu zaidi ya wengine
katika ligi ya nchini Uingereza baada ya kuondoka kwa Sir Alex Ferguson
aliyekuwa akikinoa kikosi cha Man Utd.
Arsene Wenger alitambulishwa rasmi kuwa meneja wa klabu ya Arsenal
Oktoba mosi mwaka 1996, baada ya kukamilisha mipangop ya kusaini mikataba na
viongozi wa klabu hiyo Septemba 30 mwaka huo.